Tanzania: Serikali kuendelea kukabili uvuvi haramu

BABATI 21:12:2020,

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amekemea uvuvi usiozingatia sheria na taratibu na kwamba serikali imejipanga kukomesha tabia hiyo ili raslimali zilizopo ziwe endelevu na zinufaishe kaya na taifa.

Akizungumza na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo Gekul alisema serikali itaendelea na operesheni zake za kupambana na uvuvi haramu na akataka wavuvi na wananchi washiriki katika kulinda raslimali hizo.

Mwaka uliopita Serikali ilitumia karibu Sh  bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali ili kukomesha vitendo hivyo.

“Hatutavumilia jambo hili liendelee, Sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema Gekul

Aliongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.

“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho ,” aliongeza Gekul

Aidha, Gekul alisema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia vizimba na mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa .

“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa Vijana, Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” alisisitiza Gekul

Katika hatua nyingine, Gekul aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la Serikali.

“Hili litekelezwe haraka, kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elektroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” alifafanua

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange alisema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na watayafanyia kazi kama ilivyoelekezwa ili sekta ya uvuvi mkoani humo iweze kupiga hatua inayotarajiwa.

“Tutahakikisha wavuvi wote tunawafikia kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili lakini vile vile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” alisema Twange

Mwenyekiti wa Wavuvi, Halmashauri ya Babati, Iddi Hassani alisema kuwa watafanyia kazi maelekezo na watahakikisha wanashirikiana na serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi na wataendelea kupambana na uvuvi haramu ili kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya uvuvi endelevu.

Mwisho