Tanzania: Maofisa ugani watakiwa kutoa elimu ya kilimo bora kwa kaya maskini

Singida: 13.01.2021

Maafisa Ugani wametakiwa kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya biashara  kwa kaya zote maskini nchini zinazonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

 Imeelezwa kuwa elimu hiyo itasaidia kaya hizo ziweze kupata mavuno bora yatakayoziwezesha kuboresha maisha yao na kuondokana na umaskini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akiwa kijiji cha Mtinko Wilayani Singida katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.

Ndejembi amewahimiza Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Ugani katika Halmashauri zote kutoa maelekezo kwa kaya maskini juu ya namna bora ya kulima mazao yanayostahimili ukame na kuendana na mazingira halisi ya maeneo husika ili kaya maskini ziweze kunufaika na kilimo.

“Maafisa Ugani katika ngazi ya kata na vijiji waanze kuzitembelea kaya maskini na kuzisaidia namna ya kulima kitaalamu ili ziweze kupata mavuno ya kutosha na kuongeza kuwa, Maafisa Ugani waache kwenda kwenye miradi ya nyama pekee ambayo inawanufaisha kwa kujipatia fedha”” alisema.

Sanjali na hilo, Ndejembi amepokea shuhuda mbalimbali za mafanikio waliyoyapata wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Mtinko wilayani Singida.

Mmoja wa wanufaika, Leah Ibrahimu Shila alisema, ameitumia fedha ya ruzuku aliyoipokea kujiwekea akiba kidogo kidogo na hatimaye kupata mtaji wa shilingi 200,000 uliomuwezesha kufungua mgahawa wa kuuza chakula.

Shila ameeleza kuwa, kabla ya kuwa mnufaika wa TASAF alikuwa akiishi maisha magumu yaliyomsababishia kula mlo mmoja kwa siku lakini hivi sasa anakula milo mitatu na anasomesha watoto wake katika shule za msingi na sekondari.

Naye, Zena Ramadhani Igwe amemueleza , Ndejembi kuwa, ametumia vizuri ruzuku aliyoipokea toka TASAF kwa kujenga nyumba bora ya bati kwani aliweza kuwekeza fedha kidogo kidogo ambazo zilimuwezesha kununua saruji na bati.

Ameongeza kuwa, fedha hizo zimemsaidia pia kuanza shughuli ya ufugaji wa kuku ambao wamefikia 30 na ameweza kujishughulisha na kilimo cha bustani, ikiwa ni pamoja na kumsomesha mtoto wake elimu ya sekondari.

Ndenjembi ameridhishwa na mafanikio waliyoyapata wanufaika wa TASAF, Lea Ibrahimu Shila na  Zena Ramadhani Igwe wa Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida na kutoa wito kwa wanufaika wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, kuzitumia vema fedha za ruzuku katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao na kuondokana na umaskini.

mwisho