Tani 36,298 za katani zazalishwa 2020

MUHEZA 20.01. 2021 Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mwaka 2020 uzalishaji wa mkonge nchini ulikuwa ni tani 36,298 huku malengo yakiwa ni kuzalisha tani 42,286 kwa mwaka huo.

Hata hivyo alisema katika kipindi cha 2020-2025 Bodi ya Mkonge inampango wa kuongeza uzalishaji na kufikia tani 120,000 kwa mwaka.

Alisema hayo leo wakati wa kikao cha waziri Mkuu Kassim majaliwa na wadau wa mkonge kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.

Alisema Wizara ya Kilimo itahakikisha nchi inapunguza uagizaji wa magunia ya katani kutoka nje ya nchi ili kuliongezea tija zao.

“Kwa kuanzia katika zao la korosho msimu huu wakati wa kutangaza ‘tender’ ya vifungashio tumeeleza kwamba tunatoa ‘priority’ kwa vivungashio vya katani vinavyozalishwa nchini.”

Kufuatia hatua hiyo, alivitaka viwanda vyote vya Serikali vya kutengeneza vifungashio kwa kutumia katani vilivyopewa wawekezaji binafsi kuhakikisha vinafanya kazi kwani Wizara ya Kilimo haitasita kushauri Serikali kuvirudisha Serikalini vile ambavyo havitafanya kazi kufikia mwishoni mwa mwaka fedha wa 2020/21.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saady Kambona alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020 kampuni ya mkonge ya Amboni Plantation iliongoza kwa upande wa wakulima wakubwa kwa kuzalisha tani 8,277 katika shamba la hekta 14,000 ikifuatiwa na kampuni ya Melt iliyozalisha tani 4,922.53 katika shamba lenye ukubwa wa hekta 33,000 huku wakulima wadogo nchini wakiongoza kwa kuzalisha tani 9,728.63.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao hilo linafufuliwa na tayari imefanya utafiti wa kutosha ambapo inatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 150,000 ifikapo mwaka 2025.

Wakati huo huo Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio ya kodi na tozo zote zilizopo katika zao la mkonge kwa lengo la kubaini ni zipi zenye manufaa kwa wadau na Taifa na kuainisha zisizokuwa na tija ili zifanyiwe mchakato wa kuondolewa.

Pia, Waziri Mkuu alizitaka taasisi za kifedha nchini ziendelee kuangalia kiasi cha riba kinachotozwa kwa wakulima wanaokopeshwa ili zisisababishe wahusika kushindwa kukopa kutokana na ukubwa wa riba.

Alisema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao la mkonge linarudi katika nafasi yake, hivyo aliiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kuratibu maendeleo yake kuanzia hatua za utayarishaji mashamba hadi mwenendo wa masoko.

 mwisho