Homa ya nguruwe yapiga Kanda ya Ziwa

DODOMA: 23.91.2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali imeweka mikakati  ya kuhakikisha ugonjwa wa homa ya nguruwe ulioikumba mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni unadhibitiwa.

Aidha alisema tangu ugonjwa huo uanze mpaka sasa umeshasababisha vifo vya nguruwe 1,500 wenye thamani ya shilingi milioni 375.

Ndaki aliyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuudhibiti ugonjwa huo uliokumba mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alisema kuwa vifo hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja kwa wafugaji kwa sababu kipato hicho kilichopotea ilikuwa wakipate wafugaji na akawataka wafugaji hao kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya serikali ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa kwa haraka.

Aliongeza kuwa  ugonjwa huo unaosababishwa na virusi unahama kutoka kwa nguruwe pori na  ngiri na unasambaa kupitia  njia ya maji, damu au kinyesi.

Ndaki alisema kuwa Halmashauri zilizoathirika mpaka sasa ni Mbogwe, Kyerwa, Geita, Sengerema, Kahama na Misungwi na alibainisha kuwa serikali imeshachukua hatua kadhaa za kudhibiti ugonjwa huo ikiwemo kuweka karantini.

“Tumeongeza Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Wataalamu kutoka Chuo cha Sokoine (SUA) na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwenda kuungana na wataalamu wa Halmashauri ili kuongeza nguvu ya kudhibiti ugonjwa huo,” alisema Ndaki

Ndaki alisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha wanazingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu ikiwemo kupulizia dawa za kuua wadudu kupe katika mabanda ili kuzuia ugonjwa huo usisambae zaidi.

“Niwaombe wananchi waache kula nyama ya Nguruwe, hatua hizi tunazochukua lengo lake ni kudhibiti ugonjwa usiendelee kuleta madhara zaidi katika maeneo mengine,”alisema Ndaki

Aidha, Ndaki amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi katika maeneo yaliyoathirika kuhakikikisha wanasimamia kikamilifu karantini zilizowekwa.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema kuwa ili ugonjwa huo usisambae zaidi ni muhimu wafugaji kuhakikisha kuwa mifugo yao inakuwa katika mabanda wakati wote

mwisho.