Bil 56/- zatumika kujenga vihenge vya kisasa

Njombe

Serikali ya awamu ya tano imetumia shilingi Bilioni 56 kujenga vihenge vya kisasa na maghala ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kufikia tani 501,000 mwaka 2020 toka tani 250,000 mwaka 2015.

Mafanikio hayo ya serikali yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba  wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa mkoani Njombe.

Mgumba amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli imeweza kusimamia na kutekeleza vyema ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula kwa kujenga vihenge vya kisasa na maghala.

“ Serikali imetumia Shilingi Bilioni 56 kujenga vihenge vya kisasa na maghala katika kanda nane (8) za NFRA ambapo uwezo wa kuhifadhi utaongezeka toka tani 250,000 mwaka 2015 hadi tani 501,000 mwaka 2020)” alisema Mgumba.

 “Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji na tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14,347,955” alisema Naibu Waziri Mgumba

Naibu Waziri huyo  alibainisha kuwa mahitaji yakilinganishwa na uzalishaji nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3, 511,620 za chakula ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka.

Kauli mbiu ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu inasema ‘Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu’ ambapo Serikali imedhamiria kutatua changamoto za lishe kwa kuendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multsectoral Nutrition Action Plan- 2016/2017- 2020/2021) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII) alisisitiza Mgumba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe,  Marwa Rubirya alisema mkoa wake una ziada ya chakula tani 700,000 lakini wanakabiliwa na tatizo la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano unaofikia asilimia 49.4 mwaka 2019.

 “Tumepanga kama mkoa kupambana na tatizo la udumavu kwa watoto ili tufikie angalau asilimia 33 toka 49.4 ya sasa kwani Njombe ina vyakula vingi isipokuwa hatuli vema” alisisitiza Mhadisi Marwa

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk Rashid Tamatamah alisema sekta hiyo imeendelea kukua na kuchangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama na inatoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 4.5.

Dk Tamatamah aliongeza kuwa katika mwaka 2019/20, Sekta ya Uvuvi ilikua kwa kiwango cha asilimia 1.5na kuchangia Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 1.71 ambapo uzalishaji wa samaki kutoka maji ya asili kwa mwaka 2019/20 ulifikia takribani tani 497,567 na katika uzalishaji wa mazao ya viumbe maji kufikia tani 18,716.56.

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yalifanyika mkoani Njombe na kilele kilikuwa tarehe 16 Oktoba 2020.

Mwisho.