Wasindika mchele na soko la Afrika mashariki
KAHAMA: 21.1.2021 WASINDIKAJI wa mchele wameitaka serikali kufungua soko la EAC na SADC ili waweze kuwa na bei yenye ushindani.
Imeelezwa kuwa soko la nje limebanwa na kujikuta wakigiombea wanunuzi wa ndani huku mavuno yameongezeka kutoka tani millioni 1.2 hadi tani millioni 1.8.
Wamesema wale wanaokuja kununua kutoka nje wamekuwa wakiwekewa vikwazo hivyo ni vyema wakaruhusiwa.
Wakizungumza kwenye mafunzo ya usindikaji wa zao la mpunga yaliyoandaliwa na Baraza la Mchele Tanzania (RCT) kwa kushirikiana na REPOA kupitia mradi wa Tradecom 11 unaofadhiliwa na jumuiya ya ulaya (EU).
Victor Muzo na Andrew Siria ambao ni wasindikaji wa mchele walisema kuwa mchele upo mwingi ila masoko ndiyo hayapo ila kama wangekuja wafanyabiashara kutoka nje kama Kenya na Uganda ilivyokuwa zamani wangeweza kunufaika .
Katibu tawala wilaya ya Kahama, Timothy Ndanya ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya Annamringi Macha alisema kuwa suala la kuwapata wanunuzi ni jambo jema lakini wasindikaji hao wanatakiwa waungane na wakulima katika mtandao wa ununuaji mazao nchini (TMX) kwani huko wanunuaji wataingia moja kwa moja kujua bei wanayoitaka na kununua bila usumbufu wowote.
“Na serikali haijazuia wanunuzi kutoka nje bali upo utaratibu unatakiwa kufuatwa kiusalama hivi sasa milango itafunguliwa ili wakulima waweze kunufaika siwezi kuliongelea hili hapa bado lipo kwenye utaratibu natumaini mtajulishwa hilo halina shaka” alisema Ndanya .
Ndanya alisema kuwa wasindikaji wa mchele hivi sasa sio sawa na zamani lakini uzalishaji wa zao hili bado haujachangia vyema pato la taifa kwani hekta 21 nchini zinafaa kwa kilimo cha zao hilo ambapo zinazolimwa ni hekta tisa tu ikiwa katika mkoa wa Shinyanga wilaya ya Kahama pekee ndiyo inzalisha asilimia 45 ya mchele.
Mkurugenzi mtendaji RCJ, Winnie Bashagi alisema kuwa asilimia 80 ya mchele hapa nchini hulimwa na wakulima wadogo kati ya hekta 0.2 hadi hekta 2 na hutegemewa na wasindikaji wa mchele.
“Tangu mwaka 2007 Tanzania haijaagiza mchele kutoka nje ya nchi kwani imeweka mikakati kuendeleza zao la mpunga na kulenga kuendelea kujitosheleza kwa mahitaji ya mchele na kuzalisha ziada ya kuchangia kwa kiwango kikubwa katika mahitaji ya mchele kwenye masoko ya kikanda yaani EAC na SADC” alisema Bashagi.
Bashagi alisema kuwa baraza la mchele limetoa mafunzo kwa wasindikaji 100 ili kuwajengea uwezo waweze kuzalisha mchele bora wenye viwango vinavyokidhi ushindani katika soko la ndani na nje.
mwisho