Waziri wa Kilimo aelezea vipaumbele chake
DODOMA, 21:12;2020
WAZIRI wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda amesema kipaumbele chake ni kuona wakulima wanaongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao nchini kwa kutumia eneo dogo.
Waziri wa Kilimo amesema hayo leo wakati akikakabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wizara ya Kilimo, Mtumba jijini Dodoma .
Alisema lengo ni kuwa na kilimo cha kisasa zaidi ambacho kinazalisha mazao mengi katika eneo dogo hivyo kuongeza tija na kukuza uchumi wa kaya na taifa.
“ Sekta ya kilimo inachangia asilimia 28 ya pato la taifa lakini sekta ndogo ya mazao inachangia asilimia 18 ambapo tija ni ndogo. Tija kwenye kilimo ni ndogo sana wakati theluthi mbili ya watanzania inategemea kilimo kwenye maisha ambapo asilimia karibu 70 imejiajiri huko” alisema Prof. Mkenda.
Akikabidhi ofisi Hasunga amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara ya kilimo kwa miaka miwili ya awamu yake ya kwanza.
Ili kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inaongeza kuchangia ukuaji wa uchumi toka wa sasa wa asilimia 28 hadi zaidi, Prof Mkenda alisema atahakikisha taasisi ya utafiti (TARI) na wakala wa mbegu (ASA) wanaongoza kwenye utafiti wa mbegu bora nyingi ili wakulima wazalisha zaidi.
Pia alisema atasimamia na kuelimisha mbinu bora za uzalishaji ambao utalenga kufanya umwagiliaji kwa njia ya matone ukue na kuchangia kwenye uhakika wa chakula ikiwemo upatikanaji wa viuatilifu na huduma za ugani kwa karibu zaidi .
Mkakati wa tatu Prof. Mkenda ili kukuza tija ya kilimo ni upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima kwa kusimamia masoko ya kimkakati na kufanya wakulima wanufaike na jasho lao kwa faida huku nchi ikiwa na uhakika wa chakula na malighafi kwa ajili ya viwanda vyake.
Aidha Prof Mkenda alisema katika uongozi wake ndani ya wizara ya Kilimo atahakikisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji kwenye kilimo inakuwa rahisi na wenye kunufaisha makundi ya vijana na wawekezaji .
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema kuwa wizara hiyo inazo changamoto ikiwemo kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa upatikanaji wa sukari ambapo wa sasa upungufu ni zaidi ya tani 60,000 kila mwaka na upande wa upatikanaji mafuta ya kula upungufu ni zaidi la tani 365, 000 .
Kusaya alitoa wito kwa viongozi wakuu wa wizara wapya kushirikiana na watumishi ili kuhakikisha lengo la serikali ya awamu ya tano la kufikia hekta milioni moja na laki mbili za umwagiliaji zinafikiwa na kufanya sekta hiyo ichangie zaidi kwenye ukuaji wa uchumi kwani Tanzania ina eneo la hekta milioni 29 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji kati ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo.
Mwisho.
—