Wasindika mchele na soko la Afrika mashariki

KAHAMA: 21.1.2021  WASINDIKAJI wa mchele  wameitaka serikali kufungua soko la EAC na SADC  ili waweze kuwa na bei yenye ushindani.

Imeelezwa kuwa soko la nje limebanwa na kujikuta wakigiombea wanunuzi wa ndani huku mavuno yameongezeka kutoka  tani millioni 1.2  hadi  tani millioni 1.8.

Wamesema wale wanaokuja kununua kutoka nje wamekuwa wakiwekewa vikwazo hivyo ni vyema wakaruhusiwa.

Wakizungumza kwenye  mafunzo  ya usindikaji wa zao la mpunga  yaliyoandaliwa  na Baraza la Mchele Tanzania (RCT) kwa kushirikiana na REPOA  kupitia mradi wa Tradecom 11 unaofadhiliwa na jumuiya  ya ulaya (EU).

Victor Muzo na Andrew Siria  ambao ni  wasindikaji wa mchele walisema kuwa mchele upo mwingi  ila masoko ndiyo  hayapo ila kama wangekuja wafanyabiashara kutoka nje  kama Kenya na Uganda ilivyokuwa zamani  wangeweza kunufaika .

Katibu tawala  wilaya ya Kahama, Timothy   Ndanya ambaye alikuwa mgeni rasmi  akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya  Annamringi Macha alisema kuwa   suala la kuwapata wanunuzi ni jambo jema lakini wasindikaji hao wanatakiwa waungane  na wakulima  katika mtandao wa  ununuaji mazao nchini  (TMX) kwani huko wanunuaji wataingia moja kwa moja kujua bei wanayoitaka na kununua bila usumbufu wowote.

“Na serikali haijazuia wanunuzi kutoka nje bali  upo  utaratibu unatakiwa kufuatwa kiusalama  hivi sasa  milango itafunguliwa   ili wakulima waweze kunufaika siwezi kuliongelea hili  hapa bado lipo kwenye utaratibu natumaini mtajulishwa hilo halina shaka” alisema  Ndanya .

Ndanya alisema  kuwa wasindikaji wa mchele   hivi sasa sio sawa na zamani lakini   uzalishaji wa zao hili bado haujachangia vyema pato la taifa  kwani hekta  21 nchini  zinafaa kwa kilimo cha zao hilo ambapo zinazolimwa ni hekta  tisa  tu ikiwa katika mkoa wa Shinyanga wilaya ya Kahama pekee  ndiyo inzalisha asilimia 45 ya mchele.

Mkurugenzi  mtendaji RCJ, Winnie  Bashagi  alisema kuwa  asilimia 80 ya mchele  hapa nchini hulimwa na  wakulima wadogo  kati ya  hekta  0.2 hadi hekta 2 na hutegemewa na  wasindikaji  wa mchele.

“Tangu mwaka 2007  Tanzania  haijaagiza mchele kutoka nje ya nchi  kwani  imeweka mikakati kuendeleza zao la mpunga  na kulenga kuendelea kujitosheleza  kwa mahitaji ya mchele na kuzalisha  ziada ya kuchangia  kwa kiwango kikubwa  katika mahitaji ya mchele  kwenye masoko ya kikanda yaani  EAC  na  SADC” alisema  Bashagi.

Bashagi  alisema kuwa baraza la mchele limetoa mafunzo kwa wasindikaji 100  ili kuwajengea  uwezo waweze kuzalisha  mchele bora wenye viwango vinavyokidhi  ushindani katika soko la ndani na nje.

mwisho

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *