Wakulima Pemba wapongezwa kuongeza tija kilimo cha umwagiliaji

Pemba

20.08.2020

Wakulima wa Pemba wameanza kunufaika na miradi ya kilimo inayotekelezwa kwa pamoja na serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uendelezaji zao la mpunga (ERPP) na mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC).

Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji Mpunga nchini (ERPP) umetumia shilingi Bilioni mbili  kujenga na kukarabati miundombinu ya skimu za umwagiliaji upande wa Pemba kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akizungumza wakati alipotembelea miradi ya umwagiliaji ya Ole Dodea Chake Chake na Kwalempona Wete Pemba leo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema miradi hiyo inathibitisha uimara wa Muungano uliopo .

“Nimetembelea na ninawapongeza wenzetu wa Zanzibar kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi hii ya umwagiliaji kwani wakulima wameonesha mafanikio ya kuongeza tija ya uzalishaji zao la mpunga  na pia thamani ya fedha inaonekana” alisema Kusaya.

Kusaya aliwaeleza wakulima wa Pemba kuwa miradi hiyo ya umwagiliaji ni zawadi toka kwa marais wetu ambapo amewasihi kuitunza na kuifanya iwe endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Skimu ya Umwagiliaji ya Ole Dodea Chakechake ina ukubwa wa hekta 10 maalumu kwa uzalishaji mbegu bora za mpunga na tayari wakulima 62 wameanza kunufaika kulima huku ikigharimu shilingi Bilioni 1.7 kukamilika;  wakati skimu ya Kwalempona wilaya ya Wete ina eneo la hekta 13 na wakulima 120 wengi wao akina mama wanalima mpunga na imetumia shilingi Milioni 753 kukamilika.

 “Wakulima tunzeni miradi hii na fikirieni kuanza kuchangia fedha kidogo ili mradi uwe endelevu ikitokea miundombinu imeharibika basi iwe rahisi kutumia fedha zenu kuikarabati na kupunguza utegemezi wa serikali” Kusaya aliwasihi wakulima wa Wete.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Kwalempona, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima,Shaibu Ali alisema hapo mwanzo walipata ugumu wa kulima mpunga kwenye bonde hilo kutokana na mitaro kuwa ya udongo hivyo maji mengi yalipotea lakini sasa skimu imeboreshwa .

Mkulima huyo aliongeza kusema mradi wa ERPP umesaidia wakulima kuwa na uhakika wa kulima mpunga mara mbili kwa mwaka na kuongeza mavuno toka wastani wa tani 2 kwa hekta hadi tani 5 na matumizi ya mbegu bora za mpunga.

Naye Juma Shamani Juma mkulima wa Wete alisema “ nilizoea kupanda mpunga aina ya linga na kuvuna poro 36 (  roba za kilo mia ) katika ploti yangu, lakini sasa hivi tumetumia mbegu bora na mavuno yameongezeka hadi wastani wa poro 50 ( sawa na nusu tani) kwa robo hekta” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Maryam Abdulla alisea serikali kupitia mradi wa ERPP inahamasisha wakulima kutumia mbegu bora za mpunga ili wapate mavuno mengi tofauti na mbegu za asili aina ya linga.

 “Rais Dk Ali Mohamed Shein ameagiza wizara ya Kilimo Zanzibar kutuma wataalamu kwenda Bara kwa ajili ya kujifunza namna ya kufufua zao la korosho ili wakulima wa visiwani humo wawe na zao jingine la biashara na kukuza uchumi wao” alisema Maryam

Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji Mpunga (ERPP) ulianza kutekelezwa mwaka 2015 kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 22.9  na utafikia mwisho mwaka 2021 ambapo kwa upande wa bara unatekelezwa kwa kujenga skimu 5 ,maghala 5 yamekamilika  na ujenzi wa maabara moja ya kilimo mkoani Morogoro na kwa upande wa Zanzibar jumla ya skimu 9 zimejengwa .