Jinsi Tari Naliendele inavyoanzisha kilimo cha maharage Kusini ya Tanzania

 Na Beda Msimbe

“Kiukweli kilimo cha maharage ni kipya katika maeneo hayo. Hapo zamani mazao  ambayo wakulima walizoea kulima ni karanga,njugu na mbaazi”

Maharage ni zao maarufu zaidi duniani kati ya mazao mengine ya jamii ya mikunde. Maharage yalifika Tanzania miaka mia tatu (300) iliyopita. Nchini Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika Mashariki, maharage yanazalishwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya kuuza. Mwaka 2013 Tanzania ilikuwa nchi ya sita katika uzalishaji wa maharagwe makavu duniani. Kwa mwaka huo Tanzania ilizalisha tani 1,150,000.

Nchi ya kwanza kwa takwimu za mwaka huo kwa uzalishaji wa maharagwe makavu duniani ni Myanmar ( tani 3,800,000), kifuatiwa na  India (tani 3,630,000),  Brazil ( tani 2,936,444),  China (tani 1,400,000) na  Mexico ( tani 1,294,634). Tanzania kwa mwaka huo  ilizitangulia nchi za Marekani (tani 1,110,668),Kenya ( tani 529,265),Uganda (tani 461,000) na Rwanda ( tani 438,236).

Wakulima wa Afrika mashariki wanazalisha zaidi ya nusu ya maharage yanayozalishwa barani Afrika. Nchini Tanzania, mara nyingi maharage yanapandwa pamoja na mahindi au na zao la kudumu kama ndizi au kahawa.

Pamoja na umaarufu huo wa Tanzania, mikoa ya Kusini ( Lindi na Mtwara) imekuwa mikoa migeni ya kufanya kilimo cha maharage kinachoeleweka, Wakulima wa hapa wamezoea sana kulima ufuta, korosho na kiasi fulani mbaazi, maharage kwa kubahatisha. Lakini watafiti wa Naliendele wanasema mikoa hiyo ya maeneo kusini  maharage yake hukomaa mapema zaidi kabla ya mavuno katika nyanda za juu kusini kama mikoa ya Mbeya, Iringa na  Ruvuma.

Wataalamu wa Tari Naliendele baada ya kuona kuna wakulima katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameanza kujishughulisha na kilimo cha maharage waliamua kufanya utafiti wa mbegu zinazofaa kwa maeneo hayo yanayolima maharage kwa lengo la kushauri matumizi bora ya mbegu na kilimo chenye tija.

Katika utafiti  wa kilimo kisichotegemea maji ya kumwagilia wataalamu  walilenga kupata eneo ambalo lina ardhi inayofaa kwa kilimo cha maharage kwa kuzingatia mwinuko wake kutoka usawa wa bahari. Mwinuko unaofaa kwa maharage mara nyingi ni kuanzia mita 700 mpaka 900 kutoka usawa wa bahari.

Kwa mujibu wa Dk John Tenga wa Naliendele kazi ya utafiti ilianzia kwa kuona  wanachofanya wakulima katika udogo wao wa kawaida wakilima maharage kama mboga.

Kwa kuona kwamba wapo wanaohitaji kama mboga wakati na wao wanaweza kufanya utafiti wa mimea ya mikunde ndipo walipooanza kuangalia taarifa mbalimbali za kitafiti zilizotolewa Tari Uyole ili kupata mbegu bora zinazofaa kwa mikoa ya Kusini.

Waliangalia mbegu  14 za Uyole na maeneo ambayo yanaweza kutumiwa kufanya uzalishaji kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kwa mujibu wa Dk Tenga ,mbegu ambazo walizichukua kwa ajili ya Utafiti kuona ubora wake kwa maeneo waliyoyachagua zilikuwa ni za aina 14 huku tatu zikiwa zilizokwisha pasishwa kama Pasi, Rozenda na Fibea.

“Kiukweli kilimo cha maharage ni kipya katika maeneo hayo. Hapo zamani mazao  ambayo wakulima walizoea kulima ni karanga,njugu na mbaazi” alisema Dk Tenga na kusema kwa upande wao wameshakamilisha utafiti na sasa kuanzia mwaka huu wanawaelekeza wakulima na kuona matokeo ya maelekezo yao.

” Jambo linalohitajika kukuza zao hili la maharage kuwa zao la biashara ni kufuata kanuni za Kilimo Bora cha maharage. Pili ni kwa wakulima kulima kwa wingi ili upatikanaji wake usiwe haba hicho kuchochea biashara” anasema Dk Tenga.

Anasema soko lipo wazi zaidi kwa kuwa maharage ya Lindi na Mtwara yatakuwa na soko kubwa kwa kuwa katika utafiti yameonekana kukomaa mapema zaidi kabla ya mavuno yanayofanyika nyanda za juu kusini kwenye mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Iringa.

Utafiti uliofanywa na kituo cha Tari Naliendele  ulizingatia kuhakikisha na kupeleka kilimo chenye tija kwa wakulima kwa kuwapatia mbegu ambayo inapambana na wadudu ,magonjwa yakiwemo magonjwa yanayosababishwa na fangasi, evirusi na bakajani.

Pia mbegu iliyofanyiwa kazi iliangaliwa uhakika wa hali ya hewa, ukame pamoja na kuchelewa au kuwahi kwa mvua na kuisha haraka na upungufu wa rutuba kwenye udongo. Katika upandaji wa maharage msimu huu kulikuwa na mvua kidogo na watu walichelewa nab ado walivuna.

Dk Tenga anasema baada ya kuona kwamba kuna maeneo yenye uwezo wa kuzalisha maharage yenye ubaridi kidogo yakiwa katika usawa wa mita 700 mpaka 900 toka usawa wa bahari wameanza ushawishi ulimaji wa maharage kibiashara.

Maeneo ya Mtwara kama Chilangala yako katika miinuko ya mpaka mita 900 huku maeneo ya mkoa wa Lindi yanayolima yapo katika mita 800-900 kama ya Rondo.

Katika maeneo hayo maharagwe yanachukua muda mfupi zaidi kwa mbegu zilizofanywa utafiti. “Tumepeleka mbegu 11 za utafiti na tatu zilizokuwa tayari na tumeona kwamba mbegu hizi zinafaa,” anasema Dk Tenga.

Anasema kwamba kilimo hicho kimeonesha kwamba wakulima wanaweza kuvuna tani 2.5 mpaka tatu kwa hekta moja, na kwamba kwa mikoa hiyo miwili maharage yanakomaa mapema na hata kama mvua ni kidogo.

Mwenyekiti wa zamani wa halmashauri Nachingwea, Makoroganya anasema kwamba kilimo hicho kikishika kasi kitasaidia sana wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa kwa sasa wanafuata maharagwe mikoa ya Mbeya na Ruvuma na kuuza bidhaa hiyo kwa sh 2,500 na 3,000.

“Majaribio yanaonesha mafanikio makubwa, wawekezaji waje kusaidia kuinua kilimo hiki” anasema Makoroganya na kuongeza kuwa ni jambo jema, tunahitaji kilimobiashara na hapa Naliendele wanasaidia sana.

Violet Richard ambaye ni Ofisa Kilimo Halmashauri ya Mtama anashukuru kuwapo kwa msukumo huo wa kilimo cha maharage kutokana na utafiti uliofanywa na Tari Naliendele na kusema pande hizo mbili zishirikiane kunyanyua zao hilo jipya.

Somoe Blazichochote anasema kwamba wamebaini kwamba kuna jambo jema sana katika  mbegu za Naliendele kwa kuwa katika majaribio walipewa kilo 9 za mbegu ya majaribio na wamevuna kila 69 za maharage.

Naye Jabir Mkapunda wa kijiji cha Mkopi alisema kilimo cha maharage kilichoanza kufanyiwa kazi miaka miwili iliyopita sasa kimekuwa na nguvu zaidi kwa kupanda mbegu toka Naliendele ambazo zimeonesha kufanya vyema katika maeneo yaliyochaguliwa.

Wakulima wengine Zaituni Mohamed na Halima Mwinyege wanasema wamba wanaona hatima njema ya kilimo cha maharagwe kutokana na  kuwa na mbegu bora na pia kuelekezwa kilimobiashara kinachofaa kwa mikoa hiyo.

Chuo cha  Naliendele  kiliendesha utafiti wa zao la maharage kutokana na  ukweli pia  kuwa mikoa hiyo ni karibu na soko kuu la Dar es salaam lakini pia wenyewe kwa sasa ni soko kubwa  kutokana na ulaji. 

Ukiangalia mwaka huu hadi Mei mathalani bei ya kilo moja ya maharage iliendelea kubaki sh 2,500 kwa kilo kwa mlaji  bei ambayo inahakikisha uwapo wa soko lisiyoyumba la zao hilo, mikoa hiyo ya Kusini.

Ukitazama masoko mengine unaona dhahiri kwamba  kwa muda zao hili ambalo lina matumizi makubwa miongoni mwa kaya nyingi nchini limekuwa na bei ya ya wastani katika masoko makubwa ambayo ni  Dar es salaam , Morogoro na Mara.

Soko la Dar es salaam na Morogoro bei zake kwa Machi mwaka huu zilikuwa zinapendeza kwa mkulima. Machi 4, 2020 bei ya juu kabisa ya zao la Maharagwe  ilishuhudiwa katika masoko ya mkoa wa Morogoro ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa Sh 265,000. Bei ya maharage ya gunia la kilo 100 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ilikuwa inauzwa Sh 260,000 na bei ya chini  ilikuwa ya mkoa wa Mara ya Sh 100,000.

Kwa mujibu wa takwimu za bei za jumla za mazao makuu ya chakula nchini zilizotolewa  Machi 4, 2020 na Wizara ya Viwanda na Biashara, zilionyesha kuwa bei ya maharage ya gunia la kilo 100 inauzwa Sh 260,000 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa imeshuka kutoka Sh 280,000 iliyorekodiwa juzi jijini humo.

Maharage moja ya chakula ambacho kina protini nyingi ndio mboga ya ‘serikali’ kutokana na kuwapo katika matumizi ya watu wengi wa hali ya kawaida na mi moja ya chanzo cha protini ni muhimu sana katika kujenga mwili na kuwezesha ukuaji wa mwili hasa kwa watoto na pia husaidia kutengeneza kinga ya mwili.

Kutokana na ukweli wa kutoshuka kwa bei hizo ndio maana, kilimo hiki kinaonekana cha maana sana kwa upande wa mikoa hiyo ambapo pia wataongeza idadi ya mazao wanayotumia katika  kujiimarisha kiuchumi.

Ofisa Kilimo wilaya ya Newala ……….akizungumza kuhusu juhudi za Tari Naliendele anasema kwamba ni msaada mkubwa katika kuhakikisha kwamba kuna lishe bora miongoni mwa wananchi na pia kujiimarisha kiuchumi kwa kila familia.

Mazao jamii ya kunde ambayo hujulikana kitaalamu kama Fabaceae au Leguminosae ni tunda au mbegu ya mmea huo wajamii ya mikunde na hupandwa mbegu zake, ambapo inatumika na mbegu hiyo hutumika kwa chakula, masalia hutumika kwa ajili ya mifugo, na samadi.