Walima karanga watakiwa  kubadilika kukiendesha kibiashara

Na Beda Msimbe

SONGWE: WATAALAMU  kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele, wamewataka wakulima wa karanga kubadili uendeshaji wao wa kilimo na kujikita katika kilimo biashara kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo hicho.

Wakiendesha semina mbalimbali za zao  hilo katika mikoa ya Lindi, na Ruvuma katikia mwezi wa Juni mwaka huu wamesema kwamba  matumizi sahihi ya mbegu na mawaidha ya kitaalamu kuhusu kilimo hicho kitabadili kabisa tija.

Wataalamu hao walikuwa wanafanya  elimu kupitia mashamba darasa mbalimbali waliyoshirikisha wakulima wadogo katika kupatikana kwa mbegu mpya na matumizi yake.

Mtafiti Gerald Alex wa TARI Naliendele akitoa elimu ya kilimo bora cha zao la karanga katika Siku ya Mkulima Shambani iliyofanyika kijiji Cha Ipunga wilaya Mbozi Mkoani Songwe, alisema kwamba wanataka wakulima wabadilike ili kuleta tija katika zao hilo ambalo ni chakula na pia linaweza kutengeneza mafuta.

“Tunataka wakulima watekeleze agizo la serikali katika kusaidia kupatikana kwa suluhu kwenye nakisi ya mafuta ya kupikia nchini” alisema Alex.

Alisema taasisi hiyo imepata mbegu zaidi ya 14 zilizo bora katika ukubwa, uhimili wa magonjwa na pia zenye mafuta mengi ambazo zikilimwa kibiashara zitasaidia  kukuza uchumi wa wakulima na taifa.

Alisema wakulima wamejionea wenyewe ubora wa mbegu zilizofanyiwa utafiti na sasa kinachostahili ni kuhakikisha zinafika maeneo mengi.

Fatma Ibrahim wa kutoka Kata ya Mnanje tarafa ya Maratani, wilayani Nanyumbu alishukuru mafunzo ya TARI na kusema  yamewabadili wakulima.

“Nawashukuru watafiti kwa kuja kata ya Mnanje na kutushirikisha katika zoezi kubwa la utafiti kwa mbegu.Wametukomboa kifikira na kiuchumi” alisema Fatma na kuongeza kuwa mbegu zilizoletwa zimefanya vyema katika tarafa yake.

 Naye Mariam Mohamed mkulima wa kijiji cha Holola Nanyumbu  amewataka wataalamu hao kuendelea kuwa nao kwani wamekuwa chachu ya mabadiliko.

Mkulima Mathayo Danford  anayashiriki katika kikundi cha kuzalisha mbegu za kuazimia alisema wataalamu hao wamejenga uimara wa zao hilo kwa kuwafunza kuzalisha mbegu za kuazimia.

Wakiwa Nachingwea mkoani Lindi wakulima wa eneo hilo walisema kwamba mabadiliko yanayowezeshwa na TARI yamewafanya kuamini kwamba mkombozi wao ni karanga.

Mkulima Adinani Maluka wa Nachingwea alisema kwa kufanya utafiti wa pamoja wa wakulima na wataalamu kumewafanya wananchi kutambua yanayotakiwa kuwa na tija katika zao la karanga ikiwamo kuachana na mbegu za kienyeji.

Alisema utafiti wa Naliendele haukuwapa tu mbegu bora bali na nafasi ya kutambua udongo na aina ya mbegu inayofaa kupandwa.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *