Wakulima Mvomero wanufaika na bima ya fidia ya mazao

Na Mwandishi Wetu, Mvomero

11.12.2020

Shirika la Bima la Taifa limewalipa wakulima watano wa Mvomero jumla ya shilingi milioni 23 ikiwa ni fidia ya mazao yao kuharibiwa na majanga ikiwemo mafuriko yaliyoharibu mashamba yao ya mpunga na mahindi msimu uliopita wa kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ndiye aliyekabidhi hundi ya shilingi milioni 23 kwa wakulima watano toka wilaya ya Mvomero halfa iliyofanyika leo mjini Morogoro.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Kusaya aliwapongeza wakulima hao kwa kujiunga na bima ya mazao hali inayowasaidia kujikinga na majanga ikiwemo mafuriko, ukame na wadudu waharibifu wa mazao.

“ Nimejulishwa kuwa msimu uliopita wakulima 32 kutoka wilaya tofauti hapa nchini ambao walikatia bima shughuli zao za kilimo kupitia Shirika la Bima la Taifa ,mashamba yao yaliathiriwa na majanga ,hivyo leo tunawakabidhi fedha ikiwa ni fidia kwa mujibu wa sheria na mikataba na shirika letu la bima” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema wizara yake itaendelea kuhamasisha wakulima wengi wajiunge na bima ya mazao na kulitaka shirika la Bima la Taifa kwenda mikoani.

“Nataka Mkurugenzi Mtendaji na timu yako nendeni mkatoe elimu kwa wakulima wa tumbaku wa chama cha ushirika Ukonongo wilaya ya Mlele ambao wamepata hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni moja kwa tumbaku yao kuharibiwa na mvua msimu uliopita.” alielekeza Katibu Mkuu Kusaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Dk Elirehema Doriye alisema tangu kuanzishwa kwa huduma ya bima ya mazao jumla ya wakulima 562 wamepewa kinga ambapo wengi waliokumbwa na athari wamekuwa wakilipwa fidia ya majanga.

“Zaidi ya wakulima 562 wameweza kujiunga katika huduma ya Bima ya Mazao ikijumisha wakulima wa pamba, mpunga, mahindi pamoja na pareto” alieleza Dk Doriye.

Mkurugenzi huyo wa NIC alitaja mafanikio mengine ya taasisi hiyo pamoja na kutoa elimu ya bima ya mazao na faida zake  kwa wakulima 10,716 wa mikoa ya Simiyu, Morogoro, Njombe na Iringa

Shirika la Bima la Taifa limefanikiwa pia kuanza kutoa bima ya kwa mazao ya kimkakati ikiwemo chai, tumbaku, mkonge, michikchi, cocoa, alizeti na miwa.

Mmoja wa wanufaika wa malipo ya fidia baada ya kujiunga na bima ya mazao mkulima Dorika Mlacha ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Msaidizi wa MVIWATA wilaya ya Mvomero alimweleza Katibu Mkuu Kilimo kuwa kwenye vikao vyao wakulima wengi walikuwa wakiuliza maswali mengi kuhusu faida ya bima ya mazao na kukawa hakuna majibu  lakini kwa tukio la Shirika la Bima la Taifa kulipa fidia wamepata majawabu.

“Leo nimekuwa shuhuda kuwa bima ya mazao kwa wakulima hususan waadogo ina faida kubwa . Nimefurahi sana kuona Katibu Mkuu ukitukabidhi fedha zetu fidia” alishukuru Dorika

Wizara ya Kilimo ilizindua rasmi huduma ya  Bima ya Mazao mwezi Agosti 2019 wakati wa Maadhimisho ya sherehe za Nanenane zilizofanyika mkoani Simiyu na sasa inaendealea kutoa elimu kwa wakulima