Waagizwa kusimamia uuzaji wa mbolea
Mbeya, 6:12:2020
VIONGOZI wa vijiji,mitaa na vitongoji wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameagizwa kusimamia uuzaji mbolea wenye kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali ili kuepusha wakulima kuibiwa na wauzaji wasio waaminifu.
Agizo hilo lilitolewa na Kaimu katibu Tawala wa wilaya ya Mbarali,Oliva Sule alipomwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Reuben Mfune kutoa salamu za Serikali kwenye Kikao cha kawaida cha Baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa wilayani hapa.
Sule alisema tayari jitihada zimefanyika kuhakikisha bei elekezi za uuzaji mbolea katika msimu huu wa kilimo zinafahamika kwa wauzaji na wanunuzi kwa kubandika mabando kwenye maeneo mbalimbali na kinachofuatia sasani usimamizi wa karibu.
Aliwataja viongozi wa vijiji,mitaa na vitongoji kuwa wenye dhamana kubwa ya kusimamia biashara hiyo kwakuwa wao wako karibu zaidi na wananchi ambao kimsingi ndiyo wakulima na pia wao ni rahisi kupata tarifa za mwenendo wa uuzaji bidhaa kama mbolea.
“Tushirikiane kusimamia wananchi wauziwe mbolea kwa bei elekezi ambazo zimebandikwa maeneo mengi ikiwemo maofisini.Kama kutakuwa na mabadiliko yoyote ya bei basi tutapeana taarifa kupitia njia mbalimbali lakini mtu asianze kujipangia bei zake na kuwaumiza wakulima.Na ninyi wenyeviti mnapobaini biashara imekwenda kinyume toeni taarifa mapema badala ya kuacha mpaka msimu upite ndipo mje kuanza kusema bei ilikuwa tofauti.” alisisitiza.
“Mkasimamie pia asiwepo mtu anayefanya biashara ya mbolea ya kupima…sijui kilo mbili au tatu anampimia mkulima..hapo ndipo wanapoanzia kuwaibia wananchi kwa sababu kitendo cha kuifungua tayari ujazo hauwezi kuwa sawa anaweza kufanya ujanja.Lakini pia anapoifungua na kukaa muda mrefu hata ubora unapungua.Tusimamie ni bora wakulima kama hawana uwezo wakaungana ili kununua mfuko kamili.” Alisisitiza Sule.
Kaimu katibu tawala huyo pia aliwasihi wakulima wilayani hapa kuwa makini na mbolea itakayokuwa imeganda akisema hawapaswi kuinunua kwakuwa tayari itakuwa haina ubora unaohitajika kwenye ustawi wa mimea.
Aliwaonya wafanyabiashara wenye tama ya kujipatia fedha kwa kuwaibia wakulima akisema Serikali iko macho na kwakuwa ina mkono mrefu haitoshindwa kuwachukulia hatua stahiki watakaobainika ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa,Chameta Godigodi aliwasihi wajumbe wa baraza hilo kusimamia agizo hilo akisema wakulima wengi wamekuwa wakiibiwa kwa kuuziwa pembejeo kwa bei zisizostahili huku nyingine pia zikikosa ubora.