Uzalishaji mkubwa wa mihogo uliondoa tatizo la upatikanaji wa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani

Tanzania

MWENYEKITI wa Chama Cha Wadau wa Zao la Muhogo (TACAPPA) Mwantumu Mahiza, amesema uzalishaji mkubwa wa mihogo uliondoa tatizo la upatikanaji wa futari wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema miaka ya nyuma upatikanaji wa mihogo kwenye masoko haukuwa mkubwa kama ilivyo sasa ambazo mihogo imekuwa mingi na hata bei yake ni nafuu.

“Hata upatikanaji wa futari umekuwa rahisi, mihogo imeziba pengo la ugumu wa upatikanaji wa futari” alisema.

Alisema hayo wakati wa mahojiano baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa muhogo ulioongozwa na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda.Mahiza 

Mahiza alisema endapo wakulima watahamasishwa kuhusiana na zao hilo litawasaidia kujikwamua kutoka kwenye umasikini kutokana na zao hilo kuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi hasa China.

“Nilikuwa na ekari 50 gharama ya kulima shamba na kupanda ni milioni 1.5 na kwenye kuvuna shina moja dogo linatoa hadi kilo 18 “ alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo alisema serikali itaweka kipaumbele cha kufanya utafiti wa mbegu ya zao la muhogo ili kuongeza uzalishaji kutoka tani nane hadi kufikia tani 50 kwa hekta.

Alisema kilimo cha muhogo kitakuwa na tija kubwa baada ya Taasisi ya Utafiti wa Mbegu Nchini (TARI) Kibaha, kubaini mbegu yenye uwezo wa kuzalisha tani 50 kwa hekta moja.

Pia alisema serikali itahakikisha ina imarisha masoko ya zao la muhogo .

Aliwataka wakulima kulima mihogo kama zao la biashara katika kuhakikisha wananyanyua maisha yao.

“Muhogo wa Tanzania umepata soko China, tumesaini mkataba wa itifaki kufanya biashara, soko la China ni kubwa hatutaliweza kama tutalima kidogo kidogo lakini kuunganisha nguvu kwa kuendesha kilimo chenye tija, huwezi kuondoa umaskini nchi hii kama hujawainua wakulima na kilimo ndio kinaajiri nguvu kazi nyingi,” alisema.

Alisema kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni kuzalisha mbegu zenye ubora ili ziweze kutoa matokeo makubwa.

Kwa Upande wake, Ofisa miradi wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Africa (AGRA), Donald Mizambwa  alisema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na  wakulima wa mkoa wa Kagera na Kigoma katika kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la mhongo, mahindi na maharage ili kuongeza kipato pamoja na usalama wa chakula.

“Sisi kama wadau tunaona kwamba mkutano huu utatoa ushawishi mkubwa kwa wakulima kulima muhogo kutokana na kuonesha kuna fursa
kubwa ya masoko ndani na nje ya nchi,” alisema.


Alisema katika katika mkoa wa Kagera wamefikia wakulima zaidi ya 200,000 katika mazai matatu ikiwemo muhogo na mkoa wa Kigoma zaisdi ya wakulima 170.

Mkulima na mzalishaji wa mbegu za muhogo, Gosbert Ndyamukama alisema kilimo cha muhogo kimekuwa na tija kubwa kutokana na uzalishaji kuongezeka hali inayochagizwa na uwepo wa mbegu bora.

Alisema hata masoko ya zao hilo yamekuwa mengi hali inayowasaidia wakulima kupata ari ya kuendelea na kilimo hicho.


Kwa upande wake Mkurugenzi Maendeleo ya mazao kutoka Wizara ya Kilimo Nyasebwa Chimago amebainisha malengo mengine ya Mkutano huo ni kutambua changamoto za zao la muhogo na kuzindua mikakati wa miaka 10 wa zao hilo kutokana na kutokuwa na uratibu.

Mwisho