Serikali kujenga skimu ya umwagiliaji Nguvukazi mwanavala

Songwe

Wizara ya Kilimo imesema itajenga miundombinu ya skimu ya umwagiliaji ya Nguvukazi Mwanavala katika kata ya Imalilo Songwe wilaya ya Mbarali yenye eneo linalokadiriwa kuwa hekta 6,500.

Aidha shughuli hiyo itafanyika baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa maagizo ya Rais kupitia kamati ya mawaziri.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati akiongea na wakulima wa mpunga wa skimu hiyo akiwa ziarani kukagua shughuli za kilimo.

Kusaya aliwataka wakulima wa skimu hiyo inayolimwa kwa kutumia miundombinu ya kienyeji takribani hekta 6,500 kati ya eneo lote linalofaa kwa umwagiliaji la hekta 9,500 toka mto Ruaha kijiji cha Songwe/ Ibumila ambapo wakulima wamejenga banio la asili.

“Nataka ninyi watu wa Ubaruku na kijiji cha Nguvukazi Mwanavala kitongoji cha Mnazi mfanye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji na cha kibiashara ili tupate mabilionea wengi baada ya skimu hii kujengwa miundombinu ya kisasa na serikali yenu kama alivyoagiza Rais Dk John Magufuli hivyo endeleeni kulima hapa bila hofu” alisisitiza Kusaya

Akiwa kijijini hapo Katibu Mkuu huyo alitembelea mashamba ya wakulima, kukagua mfereji mkuu uliochimbwa na wakulima wenye urefu wa kilometa 8 na pia alitembelea kiwanda cha kukoboa mpunga cha Ubaruku kinachoendeshwa na ushirika wa wakulima hao na kuahidi kutatua changamoto za upatikanaji soko la mchele.

Lengo la wizara ya kilimo ni kujenga miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima Mwanavala ili maji yasipotee bure alisisitiza Kusaya na kuongeza kuwa watalaamu wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji watahusika kufanyaka kazi hiyo baada ya maagizo ya Rais kutekelezwa.

Akitoa tarifa ya ushirika wa shamba la Nguvukazi Mwanavala Katibu wa kikundi hicho, Christopher Uhagile alisema ushirika huo ulianza mwaka 2002 na kuwa sasa una wanachama 3,500 wanaolima mpunga licha  ya miundombinu kutokuwa ya kisasa.

 “Tunamshukuru Rais Dk John Magufuli kwa maelekezo yake ya tarehe 20.12.2018 kusema tuendelee kulima eneo hili na kuwa na banio na mfereji wetu ufukuliwe na kujengwa na kuwa tusisumbuliwe tena sasa limetekelezwa na uongozi wa mkoa na wilaya” alisema Uhagile

Naye mwakilishi wa wakulima, Chubi Mbayinjini wa kitongoji cha Mnazi wilaya ya Mbarali alisema wanashukuru uamuzi wa Rais Magufuli kuondoa GN 28 haki inayowafanya waendelee na kilimo katika mashamba ya Mwanavala.

Alitoa wito kwa uongozi wa bonde la mto Ruaha ili waruhusu kibali cha kutumia maji hayo kunusuru mazao ya wakulima kipindi cha ukame na kuwezesha uzalishaji mpunga kuongezeka zaidi.

Katibu Mkuu Kilimo alikuwa kwenye ziara ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi kukagua shughuli za kilimo na kuongea na watendaji waliopo chini ya wizara ya kilimo kutatua changamoto.

Mwisho

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *