Kusaya aona ajira yenye tija kwa vijana ni kilimo

Kusaya aona ajira yenye tija kwa vijana ni kilimo

Rufiji

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya aliwahamasisha Vijana waliopata mafunzo ya kilimo na ufugaji wa kuku wa nyama na mayai kufikiria kujiajiri kwa kuanzia na mitaji midogo.

Katibu mkuu huyo alisema hayo wakati akifunga mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa vitendo kwa Vijana 48 wa mkoa wa Pwani wanaotoka  wilaya za Bagamoyo, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji.

Mafunzo yaliendeshwa kuanzia Julai hadi Desemba, 2020 kupitia Ushirika wa waliowahi kusoma Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO).

 “Kwa hali ilivyo; Serikali haina uwezo wa kuajiri Vijana wote nchini; Hiki tulichokifanya leo ni sehemu ya kuwatengenezea mazingira ili yawe rafiki kwa ninyi kujiajiri. Rais wetu wa Awamu ya Tano, Dk John Pombe Joseph Magufuli alipotamka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano; Itatengeneza ajira milioni nane (8) ni pamoja na ninyi kujiajiri kupitia Sekta ya Kilimo na Mifugo.”

“Tafuteni mikopo kwa ajili ya kuanzisha Miradi mbalimbali kupitia Halmashauri zenu kupitia mikopo ya Vijana (Asilimia 5) kina Mama (Asilimia 5) na Walemavu (Asilimia 2).”

“Undeni Vikundi na nendeni kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zenu; Mtapata mikopo na kama mtakutana na changamoto; Tutafuteni Sisi (Viongozi wenu nikiwepo Mimi Katibu Mkuu Kilimo),” alisema Kusaya.

Akijibu changamoto zilizopo katika Kituo cha kilimo cha kambi ya Vijana ya Mkongo; Katibu Mkuu Kusaya amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Wizara ya Kilimo kufika katika Kituo cha Mkongo ili kufanya tathmini ya kuboresha mfumo wa maji kutoka Mto Rufiji.

Katibu Mkuu pia amemueleza Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO kuleta maombi rasmi  ya kuboreshewa bwalo la chakula, mabweni ya Vijana wanaolala Kituoni wakati wa kupata mafunzo.

Aidha, Kusaya ameahidi muda mfupi kuanzia leo kukipa Kituo cha Mkongo, trekta dogo (Power Tiller) jipya, pikipiki mbili mpya pamoja na kutoa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa banda bora la kufuga kuku pamoja na kununua kifaa cha kutotoresha vifaranga (Incubator)

Mafunzo hayo yaliendeshwa katika kambi ya Vijana iliyopo katika kijiji cha Mkongo, kata ya Mkongo wilayani Rufiji ambapo sehemu ya mafunzo hayo ilikuwa ya vitendo kwa asilimia 80 na nadharia kwa asilimia 20.

Katika taarifa yake kwa Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO Revocatus Kimario amesema; Wahitimu wamepata nafasi ya kujifunza namna bora ya kulima mazao ya bustani (Mbogamboga na Matunda), mafunzo ya kufuga kuku wa nyama na mayai, mafunzo ya utengezaji wa vyakula vya mifugo (Kuku wa nyama na mayai).

Naye muhitimu wa mafunzo kutoka Mkuranga, Wisdom Samson alitoa ombi kwa niaba ya Wahitimu wenzake 48 kupewa ardhi kwenye Halmashauri zao pamoja na mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara za ufugaji na kilimo pia kusaidiwa kudhaminiwa ili kupata mikopo ya bei nafuu kutoka  Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO, Revocatus Kimario amemweleza Katibu Mkuu Kusaya kwamba Taasisi yao imekuwa ikitumia Kituo cha Mafunzo Mkongo kuanzia mwaka 2015 na kwamba tayari imetoa mafunzo kwa Vijana zaidi ya 1,461.

Mwisho.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *