Kilimo kupitia upya Sheria ya Ushirika

Dodoma: 06.01.2021 WIZARA ya kilimo imesema inajipanga kuanza kupitia upya Sheria ya Ushirika  na kupata maoni ya wadau ili kuwa na sheria mpya ya Ushirika itakayoendana na mazingira ya sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda wakati wa halfa ya kukabidhi magari, kompyuta na Laptop  kwa Warajisi Wasaidizi wa mikoa ya Tanzania Bara, mjini hapa.

Alisema upitiaji huo  ni sehemu ya mikakati ya wizara yake kuhakikisha heshima na hadhi ya sekta ya ushirika inarejeshwa kama ilivyokuwa miaka ya mwanzoni mwa uhuru wa Tanzania Bara.

Alisema enzi hizo ushirika uliweza kujiendesha na kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi.

 “Kuna maendeleo makubwa kwenye ushirika lakini tuna kazi ya kuhakikisha tunarudisha heshima na hadhi ya ushirika wenye uwezo na nguvu ya kutafuta masoko ya mazao ya wakulima na kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi kama ilivyokuwa miaka ya 1950” alisema Prof. Mkenda

Prof. Mkenda  alisema pia ni nia ya wizara yake kudhibiti wizi na ubadhirifu wa mali za wana ushirika ambapo amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia Kamati Maalumu ya kufuatilia na kurejesha mali za ushirika zilizokuwa zimeporwa na kuuzwa kinyume cha utaratibu na sheria.

Aidha alisema wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika itawajengea uwezo watumishi wake ili waweze kuratibu na kusimamia sekta ya ushirika kwa weledi zaidi.

Kwa upande wake Mrajis wa Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dk Benson Ndiege alisema wamefanikiwa kununua magari manne kwa gharama ya Shilingi milioni 275 zilizotokana na bajeti yao ili kuwezesha uratibu na usimamizi wa kazi mikoani.

Magari hayo manne mapya yamegawiwa kwa Warajis Wasaidizi wa Mikoa ya Kilimanjaro, Simiyu, Njombe na Dar es Salaam na pia Tume imetoa gari moja jingine kwa Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Kigoma ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa mwezi Desemba 2019 alipofanya ziara mkoani Kigoma ili litumike kusimamia na kuhamasisha kilimocha michikichi kwenye AMCOS .

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda (kulia) akikabidhi gari kwa Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, John Henjewele (kushoto) kwenye hafla iliyoanyika mkoani Dodoma juzi. Gari hilo ni moja kati ya manne yaliyonunuliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa gharama ya shilingi milioni 275. (Picha na Wizara ya Kilimo)