Katibu Mkuu ataka weledi na uadilifu watumishi Kilimo
Morogoro
Watumishi wa Wizara ya Kilimo wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
Wito huo umetolewa leo mjini Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati alipofungua mafunzo ya siku nne kwa wakuu wa taasisi, bodi na wakala chini ya wizara kuhusu kamati za kudhibiti uadilifu.
Kusaya amewataka watumishi wote kuwa waadilifu ndani ya mioyo yao ili watende kazi walizokabidhiwa bila upendeleo na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Lengo la wizara ya kilimo ni kuwa na watumishi wenye uadilifu na maadili mema ndio maana nimetoa kibali mafunzo haya yafanyike na kuwezesha kutimiza malengo ya kazi . Mtumishi mwadilifu atatumikia watanzania muda wote “alisema Kusaya
Mafunzo haya yanawakutanisha wakuu wa taasisi, bodi za mazao na wakala pamoja na kamati za uadilifu toka taasisi zote 23 chini ya wizara ya kilimo.
“Tujione tunawiwa kuwahudumia watanzania kwani tumepewa dhamana ya kuwatumikia wenzetu kwa uaminifu na uadilifu “alisema Kusaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala Udhibiti wa Viuatilifu (TPRI), Dk Magret Mollel amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutoa kibali cha kufanyika mafunzo hayo yenye kulenga kuongeza tija na utendaji kazi wa wizara ya kilimo.
Dk Mollel alisema kwa siku nne wajumbe wa kamati za uadilifu toka taasisi zote za wizara watashiriki mafunzo ya uadilifu na maadili toka kwa wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais Utumishi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Kilimo Filbert Lutare alisema mafunzo hayo yanahusisha washiriki 130 toka taasisi 23 chini ya wizara; na kuwa wizara itahakikisha baada ya mafunzo haya watumishi kwenye taasisi zote wanaishi uadilifu na kuongeza kiwango cha maadili mema katika kuhudumia umma. Aliongeza kusema kuwa Kamati za Kudhibiti Uadilifu zinaundwa kwa mujibu wa Waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi wa mwaka 2017 ukilenga kutekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu ili watumishi wa umma washiriki kikamilifu na kwa vitendo kupambana na vitendo vya rushwa.