Kampeni ya “ondoa mapori ongeza uzalishaji” yapamba moto Mtwara


Na Mwandishi Maalumu, Mtwara

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Mtwara, imetoa mafunzo ya namna ya kubebesha vikonyo vya mikorosho katika mikorosho iliyozeeka kwa wakulima wa kata ya Madimba mkoani Mtwara ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya “ondoa mapori ongeza uzalishaji” yenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija kwa zao la korosho mkoani Mtwara.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na  Mratibu na mtafiti wa zao la korosho, Dk Geradina Mzena kutoka Tari Naliendele mkoani Mtwara.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika Shamba la shule ya Msingi Mtendachi mtaalamu huyo aliwaonesha wakulima namna bora ya uondoaji wa mikorosho ya zamani, namna ya kuikata ili ipate maoteo mapya, upachikaji (ubebeshaji ) wa vikonyo sambamba na utoaji wa elimu ya upandaji na utunzaji wa mikorosho.

Alisema kwamba taasisi yake ipo tayari kutoa mafunzo hasa kwa maofisa ugani  ili waweze kuwa na uelewa mkubwa wa kusaidia wakulima wao.

“Tunawaomba maofisa ugani kuwa na orodha ya wakulima wao, wakawasaidia maandalizi na kufika Naliendele kuchukua vikonyo vya miche bora ili kuibebesha katika maoteo ya mikorosho ya zamahi” alisema Mzena.

Aidha aliwataka wakulima kuhakikisha kwamba wanapanda mikorosho mipya inayotokana na mbegu bora zilizozalishwa na Tari naliendele ili kuwa na tija kubwa.

Wakulima waliohudhuria mafunzo hayo  kwa vitendo katika shamba hilo,wamesema kwamba  ni zoezi bora kabisa ambalo hawajawahi kulipata na kutaka taasisi hiyo kurejea kila mara kuhakikisha kwamba kuna uelewa wa juu wa kampeni ambayo lengo lake ni kuongeza tija.

Musa Kitenga mkazi wa  Nandondi  alisema kwamba uhamasishaji wa kilimo hicho wenye kwenda sanajari na mafunzo umemweka katika hali nzuri zaidi ya kuondoa pori katika shamba lake na kuweka mikorosho mipya yenye tija.

Alisema utaalamu aliopewa katika mafunzo hayo kw amsaada wa maofisa ugani ataupeleka katika shamba lake.

Shamba hilo la shule nui miongoni mw amashamba kadha yaliyoanzishwa na Tari Naliendele mwaka 1984 ikiwa na mikorosho na kukabidhiwa kijiji ambacho nacho kilikabidhi kwa shule.

Alisema mafunzo ya ubebeshaji vikonyo ni mafunzo yenye manufaa makubwa na kutaka kuwepo na  uhamishaji wa maarifa hayo wka wakulima.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nandondi, kata ya Madimba , tarafa ya Ziwani  Said Mdabwa alisema hana shaka kwamba zoezi hilo lina manufaa makubwa kwa uchumi wa kaya moja moja, kijiji hadi taifa.

“Nawashukuru Tari Naliendele kwa kuleta elimu hii ambayo itaongeza tija kwa wakulima na hivyo kuvuna  korosho nyingi zaidi” alisema Mdabwa.

Alisema kijiji hicho chenye wakazi 2,800 itasaidia kuondoa mapori na pia kuwa na uelekeo mpya wa kushughulikia zao la korosho ili kuwa na mazao mazuri kwani zao hilo ambalo ndio msingi wa uchumi wa kijiji na kata hiyo.

Mwenyekiti wa Shule ya msingi ya  Mtendachi, Mohamed Ngome  amesema mafunzo na kazi iliyofanyika katika shamba hilo la shule itasaidia kuongeza tija na  mapato ya shule hiyo na hivyo kupunguza mzigo kwa wazazi.

Ofisa Kilimo  kata ya Madimba, Nico Lukoya alisema kwamba  amefurahishwa na jinsi wakulima walivyojitokeza kupata elimu hiyo ambayo itaongeza tija zaidi katika  kilimo cha korosho.

Alisema pamoja na mafunzo hayo wakulima wa Madimba pia wanafanya mabadilio katika michezo yao kwa kupata miche bora ya korosho iliyoletwa na serikali ambayo huuzwa kwa wakulima kwa bei nafuu ya sh 500  kwa mche.

Desemba 16, 2020 Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa, alizindua rasmi kampeni ya kuhamasisha upandaji wa mikorosho mipya yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la korosho katika Mkoa wa Mtwara akiita “ondoa mapori ongeza uzalishaji”.

Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *