Agricom, NBC wakubaliana kusaidia wakulima wadogo wa mkonge

Na Beda Msimbe

TANGA:KAMPUNI ya wauzaji wa pembejeo za kilimo AGRICOM  na Benki ya NBC weameingia makubaliano yatakayowezesha wakulima wadogo kukopa zana za kilimo cha zao la mkonge na hivyo kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao.

Akizungumza katika Maonesho ya utendaji kazi wa zana za kilimo Wilayani Korogwe yaliyoandaliwa na Agricom kwa ajili ya wakulima wa zao la mkonge hivi karibuni, Meneja wa Agricom kanda ya Kati , Peter Temu alisema lengo la kuwa na maonesho hayo ni kuwaelimisha wakulima kuhusu zana mbalimbali wanazoweza kuzipata katika kampuni yao  kupitia benki ya NBC.

” Kuna jitihada kubwa za serikali kuwekeza katika zao la mkonge na kwa kulitaja kama zao la kimkakati nchini litakaloweza kukuza uchumi wa wakulima, limetufanya na sisi kuja kuchangia kwani tunaona bado wakulima  wana changamoto ya zana duni za kilimo na hivyo kupunguza  tija ya zao ” alisema Temu na kuongeza kuwa wamesogeza huduma wilayani humo ili kurahisisha upatikanaji wa zana bora zitakazoongeza thamani ya zao hilo sokoni.

Temu alisema kwamba kwenye maonesho hayo wameopeleka mahitaji halisi ya wakulima ikiwamo matrekta aina ya Swaraj 855 lenye kokota jembe na Swaraj 963 lenye trela la kubebea bidhaa kama mkonge kutoka shambani.

Akizungumza katika halfa hiyo Ofisa Ushirika Mwandamizi wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe, Odilia Kitia alishukuru kampuni ya Agricom kwa kuona fursa katika wilaya yake na hivyo kuitumia kuinua kilimo cha mkonge kuwa cha kisasa zaidi.

Alisema ili kuwepo na uhakika wa tija ni lazima wakulima waondokane na kilimo cha mkono na utunzaji wa zao hilo kwa kilimo cha mkono na ujio wa kampuni hiyo na Benki ni kitu cha kufurahisha sana.

Naye Meneja wa Biashara wa NBC Tanga, Aljiran Mbwani akizungumza katika mkutano alisema kwamba wamekubaliana na Agricom kuwezesha mikopo ya zana za kilimo kwa wakulima ambao sharti ni kuwa na shamba la ekari 20 na kuendelea kwa wanaoataka matrekta.

“Mikopo yetu haina masharti zaidi ya kuwa na shamba la ekari 20 na uzoefu wa miaka 3 na akaunti ya NBC unayopitishia mauzo ambapo tutaona namna ambavyo tunaweza kukata deni la mtambo uliokopa” alisema Mbwani.

Alisema mikopo hiyo inalipwa mpaka miaka mitano na inawahusu wakulima walio katika vikundi vya ushirika kama Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha mazao (AMCOS) cha Mwelya ambako ndiko shughuli ilipofanyika, Hatibu Majaliwa aliwataka wakulima kutumia fursa ya mikopo kubadili kilimo chao kuwa cha kisasa ili kiweze kuwa na tija.

Hata hivyo aliishukuru serikali kwa kuliwezesha zao la mkonhge kuwa zao la kimkakati ili kulisukuma kuwa na tija na kufungua fursa ya kuilimo biashara.

Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao ya Mkonge Bodi ya Mkonge Tanzania, Olivo Mtung’e aliitaka kampuni ya Agricom kuanzisha vituo vya huduma ili kuhakikisha kwamba wakulima wanatumia zana walizonazo kwa lengo la kuongeza tija.

“Naamini ujio wa Agricom utakuwa chachu kubwa ya kuimarisha kilimo cha mkonge katika halmashauri ya korogwe” alisema Mtung’e.

Mmojawapo wa wakulima wa mkonge, Rabihimju Shekwavi alishukuru kampuni ya Agricom kwa kuona umuhimuwa kuwaletyea zana za kubadili kilimo chao ambacho kilishindwa kusonga mbele kutokana na kutegemea jembe le mkono pekee.

msimbebeda@gmail.com
Imehaririwa na Anthony Muchoki