AGCOT: Utekelezaji wa Maono ya Rais Samia kwa Mapinduzi ya Kilimo

Dodoma, Tanzania – Aprili 27–28, 2025

Katika hatua ya kihistoria kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Mpango wa Maendeleo ya Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), tukio lililoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na kufuatiwa na ziara ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika banda la AGCOT kwenye uzinduzi wa Coop Bank , Dodoma.

Kutoka SAGCOT hadi AGCOT: Tanzania Yajitanua Kwenye Kilimo cha Kibiashara

AGCOT ni mwendelezo na upanuzi wa mpango uliothibitishwa wa SAGCOT, unaojumuisha sasa shoroba nne za kilimo:

  • SAGCOT Corridor (Kanda ya Kusini)
  • Mtwara Corridor (Lindi, Mtwara, Ruvuma)
  • Central Corridor (Dodoma, Singida, Tabora, Kanda ya Ziwa)
  • Northern Corridor (Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga)

Mpango huu unalenga kuchochea uzalishaji wa mazao kwa tija, kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko, na kuwezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kilimo.

Ziara ya Mheshimiwa Rais: Uthibitisho wa Dhamira ya Juu

Katika ziara yake ya tarehe 28 Aprili 2025, Mheshimiwa Rais Samia alielezwa kwa kina kuhusu mafanikio ya SAGCOT na upanuzi wake kupitia AGCOT. Alikutana na vijana waliofanikiwa kama Raha Vegetable Farm, anayezalisha miche ya nyanya, na Get Aroma, kampuni ya viungo, waliothibitisha kuwa kilimo kinalipa kupitia usaidizi wa AGCOT na mpango wa BBT.

Mheshimiwa Rais alisisitiza umuhimu wa kuongeza usindikaji wa mazao, kuwa na masoko ya ndani na nje, na kuwekeza katika miundombinu bora ya kilimo vijijini.

Hatua Zinazofuata na Mwelekeo Mpya

  • Kuanzishwa kwa Kanda Maalum za Usindikaji wa Mazao (SAPZs)
  • Uendelezaji wa miundombinu ya masoko, barabara, maji, umeme
  • Ushirikiano wa karibu chini ya Agriculture Transformation Office (ATO)
  • Kuandaa mpango wa uwekezaji maalum kwa kila shoroba

Umuhimu wa Wadau Wote

AGCOT inapaswa kubaki jukwaa huria – lisiloegemea upande wowote wa kisiasa wala kiutendaji – bali lifanye kazi kwa usawa kwa Serikali, sekta binafsi, vyama vya ushirika, taasisi za utafiti na wakulima wadogo. Ushirikiano huu wa kina ndio msingi wa mafanikio ya AGCOT.

Hitimisho: Tanzania Mpya Kupitia Kilimo Biashara

AGCOT ni chombo cha kimkakati cha kufanikisha Dira ya Maendeleo ya 2050, kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kupitia kilimo hadi Dola Bilioni 100, na kuongeza mauzo ya nje ya mazao hadi Dola Bilioni 20. Mpango huu unalenga kuchochea maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote – kutoka shamba hadi soko, kutoka kijiji hadi masoko ya kimataifa.

Kaulimbiu: “Tukuze Kilimo Endelevu, Tulishe Afrika na Dunia.”



Add a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *