Tanzania inaendelea na udhibiti wa ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea waliovamia mashamba katika wilaya 22 zilizopo kwenye mikoa 12 nchini
DODOMA:13.5.2021
SERIKALI imesema inaendelea na udhibiti wa ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea waliovamia mashamba katika wilaya 22 zilizopo kwenye mikoa 12 nchini.
Kazi ya kudhibiti ilianza Novemba 17 , 2020 na bado inaendelea.
Aidha imesema kwamba kazi ya kudhibiti ndege hao inaendelea pia katika maeneo mapya yaliyoripotiwa katika Mkoa wa Tabora na Simiyu na maeneo ambako yalishadhibitiwa lakini makundi mapya ya kwelea yameanza kujitokeza Wilaya ya Mbarali (Mbeya), Babati (Manyara) na Kishapu (Shinyanga).
Mikoa ambayo imevamiwa na wilaya zake katika mabano ni Kilimanjaro (Mwanga, Moshi), Arusha (Wilaya ya Meru), Manyara (Simanjiro na Babati), Dodoma (Chamwino, Bahi, Kondoa, Dodoma Jiji), Singida (Singida Vijijini, Itigi, Mkalama), Morogoro (Kilosa na Mvomero), Iringa (Iringa Vijijini), Mbeya (Mbarali), Geita (Geita Vijijini), Mwanza (Sengerema na Kwimba) na Shinyanga (Kishapu na Shinyanga Vijijini) na Pwani (Chalinze).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusu juhudi za serikali kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao , Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda alisema pamoja na hatua hizo zinazochukuliwa pia amelihakikishia taifa kwamba hakuna tishio la nzige wa jangwani baada ya kazi kubwa ya kukabiliana nao kwenye eneo la jumla ya hekta 6,441 nchini.
Kazi hiyo ya kupambana na nzige hao waliovamia wilaya ya nane wakitokea nchi jirani ya Kenya ilifanyika kuanzia Machi 4, 2021 hadi Aprili 13, 2021 na kwamba mpaka sasa haijabainishwa uwepo wa nzige au tunutu walianguliwa .