Waziri wa Kilimo Prof Mkenda aeleza vipaumbele vyake
Dodoma
Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda amesema kipaumbele chake ni kuona wakulima wanaongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao nchini kwa kutumia eneo dogo kuzalisha mazao mengi zaidi na kukuza uchumi wa kaya na taifa.
Waziri wa Kilimo amesema hayo wakati akikabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga katika hafla iliyofanyika makao makuu ya wizara Mtumba jijini Dodoma .
Hafla ya makabidhiano imefanyika kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dk John Magufuli kumteua Prof. Mkenda kuwa Waziri wa Kilimo katika awamu hii ya pili ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano.
“ Sekta ya kilimo inachangia asilimia 28 ya pato la taifa lakini sekta ndogo ya mazao inachangia asilimia 18 ambapo tija ni ndogo. Tija kwenye kilimo ni ndogo sana wakati theluthi mbili ya watanzania inategemea kilimo kwenye maisha ambapo asilimia karibu 70 imejiajiri huko” alisema Prof. Mkenda.
Katika salamu zake Hasunga amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara ya kilimo kwa miaka miwili ya awamu yake ya kwanza na kuwa alifanya kazi kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula.
“Nimefanya kazi miaka miwili kama Waziri wa Kilimo, nafurahi katika kipindi chote cha kwanza cha awamu ya tano nchi imeweza kujitosheleza kwa chakula” alisema Hasunga.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema atahakikisha sekta ya kilimo inaongeza kuchangia ukuaji wa uchumi huku akitaja mambo makuu manne ambayo ni dira kwake wakati akiongoza Wizara ya Kilimo.
Kwanza kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia eneo dogo kuvuna mazao mengi hivyo taasisi ya utafiti (TARI) na wakala wa mbegu (ASA) lazima ziwe kazini muda wote kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Pili, kusimamia na kuelimisha mbinu bora za uzalishaji (Good agricultural practices) ambapo amelenga kufanya umwagiliaji kwa njia ya matone ukue na kuchangia kwenye uhakika wa chakula ikiwemo upatikanaji wa viuatilifu na huduma za ugani kwa karibu zaidi.
Mkakati wa tatu Prof. Mkenda ni upatikanji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima huku nchi ikiwa na uhakika wa chakula na malighafi ya kutosha.
Nne, atahakikisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji kwenye kilimo ili kunufaisha vijana na wawekezaji
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema wizara hiyo inazo changamoto ikiwemo kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa upatikanaji wa sukari ambapo wa sasa upungufu ni zaidi ya tani 60,000 kila mwaka na upande wa upatikanaji mafuta ya kula upungufu ni zaidi y a tani 365, 000 .
Kusaya alitoa wito kwa viongozi wakuu wa wizara wapya kushirikiana na watumishi ili kuhakikisha lengo la serikali ya awamu ya tano la kufikia hekta milioni moja na laki mbili za umwagiliaji zinafikiwa.
Tanzania ina eneo la hekta milioni 29 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji kati ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo hicho.