Vyakula vyawasilishwa kusaidia wanafunzi kusoma kikambi

NACHINGWEA: 22:7:2019 MKUU wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka wadau wa elimu mkoani humo kusaidia mahitaji ya kambi za ‘mada tata’ kusaidia juhudi za serikali kuinua elimu katika mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Rukia Muwango wakati akipokea msaada wa vyakula mbalimbali kwa ajili ya kambi 74 za madada katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi.

Msaada huo ambao umetolewa wiki iliyopita na Chama Kikuu cha Ushirika cha wilaya za Nachingwea,Liwale na Ruangwa cha Runali umetolewa kuongeza nguvu katika kambi hizo zinazoandaa watoto wa darasa la saba.

Mkuu huyo wa mkoa alitaka wadau mbalimbali wakiwamo wazazi, vyama vya ushirika vya msingi kushirikiana na serikali katika kuimarisha matokeo ya shule za msingi kwa kuboresha uelewa kabla ya mitihani.

Alisema kitendo kilichofanywa na Runali ni kitendo cha kizalendo, kwani wameunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakuwa na uelewa mkubwa kabla ya kuingia katika mitihani yao.

Akikabidhi msaada huo wenye thamani ya zaidi ya sh milioni 7, Mwenyekiti mwa chama cha Runali, Hassan Mpako alisema kwamba wamefanya hivyo kutekeleza moja ya kanuni za ushirika za kurejesha faida kwa umma.

“ Bodi ya chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kwa kuona umuhimu wa suala la elimu imeamua kutoa kidogo ilichonacho katika sekta ya Elimu kwa Wilaya zetu ambazo tunazihudumia za Ruangwa, Nachingwea na Liwale.” Alisema Mpako.

Mpako aliongeza kuwa:“Tunaomba vyama vya msingi kutupia jicho kwenye makambi hayo ili yaweze kutekeleza yale malengo waliyojiwekea ya kupata ufaulu mzuri.”

Wilaya hizo zinaendesha makambi kwenye kata zake zote 73 na kwa wilaya ya Nachingwea ina kambi pia la kiwilaya hivyo kufanya jumla ya makambi hayo kuwa 74.

Akitoa mchanganuo wa msaada huo, msomaji wa risala Carolina Samwel alisema kwamba wilaya ya Nachingwea imepatiwa mchele Kilo 1,360 sawa na mifuko 34 yenye uzito kilo 40 kila kimoja, maharage kilo 340 sawa na mifuko 34 na lita 170 za mafuta ya kupikia sawa na dumu 34.

Wilaya ya Ruangwa ilikabidhiwa kilo 800 za mchele sawa na mifuko 20, maharage kilo 200 sawa mifuko 20 na mafuta ya kupikia lita 100 sawa na dumu 20.

Aidha Wilaya ya Liwale imekabidhiwa kilo 800 za mchele sawa na mifuko 20, maharage kilo 200 sawa na mifuko 20 na mafuta ya kupikia lita 100 sawa na dumu 20.

Maofisa wa elimu Msingi kutoka wilaya hizo, Mrope (Ruangwa), Bulengwa (Nachingwea) na Mhagama (liwale) wamesema kwamba msaada huo ni kitu cha maana katika historian a kwmaba umekuja wakati muafaka.

Walisema moja ya matatizo ya kambi hizo za mada tata ni chakula na kusema msaada wa Runali ni wa kuigwa.

Naye mwalimu Hassan Mpwapwa, mwalimu mkuu wa shule ya Mianzini alisema pamoja nay eye kuwa mtoa mada katika kambi hizo, wadau wanasrtahili kuchangia chakula kwa kuwa ni tatizo kubwa.

Naye Mrajis wa Ushirika mkoa wa Lindi, Roberty Msunza alisema kwamba moja ya kanuni za ushirika ni kusaidia wananchi na kusema kitendo cha Runali kinafaa kuigwa na vyama vyote vya ushirika.

Alisema mkoa huo una vyama vya msingi 250 na kama kila kimoja kikitoa msaada wake, wanafunzi haow atasoma kw autulivu na hivyo kuongeza ufaulu.

Chama kikuu cha ushirika RUNALI kilianzishwa baada ya kuvunjika chama kikuu cha ushirika ILULU mwaka 2013 kikiwa na wanachama waanzilishi 52 na hivi sasa kina vyama wanachama wapatao 104.

Kazi kubwa ya chama hicho ni kukusanya, kusindika na kuuza mazao ya wakulima kupitia vyama wanachama kwa lengo la kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya maisha ya wanachama na wakulima kwa ujumla, ili kuongeza kipato chao kupitia vyama vyao vya ushirika vya msingi (Amcos).