Tanzania: Waliosababisha ‘dhiki’ kuzuiwa kuwania uongozi Ushirika

LINDI: 22:12:2020

Msajiri wa vyama vya Ushirika Lindi, Edmund Massawe ameonya viongozi wa vyama vya ushirika waliosababisha hasara katika vyama vyao kutothubutu kuchukua fomu za kuwania uongozi.

Akizungumza baada ya mnada wa kumi wa korosho wilaya ya Liwale hivi karibuni, Masawe alisema kwamba vyama vya ushirika hasa vya mazao vinatarajia kuanza uchaguzi wiki ya Pili ya Januari mwakani na kwamba baadhi fomu zimeshaanza kutolewa.

Msajiri wa vyama vya Ushirika Lindi, Edmund Massawe

Alisema katika juhudi za serikali kuimarisha ushirika, safari hii waombaji hasa kwenye vyama ambavyo vimesababisha hasara au vina mapungufu makubwa wanachama wake watachambuliwa vilivyo na vyombo vya serikali.

“Tutashirikiana na  serikali kufanya upembuzi yakinifu wa waombaji hasa katika vyama vyenye matatizo makubwa, hasara na havina uelekeo au vimesababisha hasraa kwa wakulima ama chama kikuu” alisema Mrajis.

Alisema;” vipo vyama vimekusanya  bidhaa bila kufuata utaratibu na kuharibu soko kwa kuwa bidhaa ni chafu, wanaomba uongozi huko lazima tuwachambue sana.”

Alisema  vyama vya ushirika vya mazao anavitarajia kuanza uchaguzi baada ya Januari 15 ingawa Saccos zitaanza mapema.

Akizungumzia uchaguzi wa Vyama Vikuu vya ushirika, alisema Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kinastahili kuanza kujiandaa kwa uchaguzi mwakani kwa kuwa minada yake ya korosho imeisha iliyobaki ni midogo.

“Lindi mwambao wamemaliza mnada wa kumi  hivi karibuni kwa sasa wanaweza kabisa kujiandaa kwa uchaguzi mwakani” alisema Massawe na kuongeza kuwa wanaowania uongozi katika chama hicho ni lazima wajue kinachowasubiri.

Alisema kwamba  chama hicho hakina mali kama maghala na mengineyo yanayotoa nguvu kwa wanachama hivyo viongozi wajao itabidi wajifunge mikanda kutengeneza miradi itakayowawezesha kuhudumia wanachama wao.

Alisema kwamba chama kama cha RUNALI kina mali mbalimbali yakiwemo maghala. Mali hizo zinasaidia sana kutotegemea wakulima katika shughuli za maendeleo za chama.