Tanzania: Walima choroko watakiwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani

Shinyanga: 11.1.2021 MAOFISA kilimo mkoani Shinyanga wametakiwa kutoa elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima wa zao la choroko ili waache tabia ya kuuza mazao yakiwa bado shambani .

Imeelezwa kitendo cha kuuza mazao hayo yakiwa shambani kunanufaisgha walanguzi wakati wao wanabaki maskini.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Zainab Telack wakati wa ufunguzi wa kikao cha siku moja kilichowakutanisha  wadau wa zao la choroko Mkoani Shinyanga.

Kikao hicho kililenga kujadili namna bora ya matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kuhakikisha unaleta tija kwa wakulima wa zao hilo na taifa kwa ujumla.

Aidha Bi. Telack aliongeza kuwa kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani itawezesha wanunuzi wa zao hilo kuwa na uhakika wa eneo la kupata mzigo mkubwa kwa wakati mmoja.

Bi. Telack aliongeza kuwa ni agizo la serikali kuhakikisha mazao ya aina ya kunde yanatumia mfumo stakabadhi ghalani kama ilivyo kwa zao la korosho.

 ‘’Nataka kuona wakulima Mkoani Shinyanga wakiwa na uwezo wa kusomesha watoto, kujenga nyumba bora na kufaidika na jasho lao sio mkulima analima mpunga katika maji mengi lakini mnunuzi ananunua mpunga bado ukiwa shambani nakuvuna gunia sitini kwa kumlaghai mkulima kwa kumpatia bodaboda.’’alisema Bi. Telack.

Aidha Bi. Telack alimwagiza Kaimu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga Bi. Hilda Simon kukutana na viongozi wa vyama vya msingi na Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga(SHIRECU) kuweka mikakati ya pamoja ya kutoa elimu kwa wakulima ili wajue faida ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Naye Kaimu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga Bi. Hilda Simon alisema kuwa changamoto ya kushindwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani inapelekea kushindwa kuwa na takwimu sahihi za zao hilo, kuendelea kuwepo kwa utoaji vibali holela vilivyokuwa vikitolewa na Halmashauri bila kupitia vyama vya Msingi.

Bi. Hilda aliongeza kuwa vibali hivyo vilikuwa vikitolewa kwa wanunuzi wa kati ambao kimsingi ndio wapinzani wa mfumo wa stakabadhi ghalani na hivyo kuendelea kunyonya mkulima kwa kununua choroko kwa bei za chini.

mwisho