Sintofahamu uzalishaji wa mpunga kapunga yamalizwa

MBARALI 8.7.2018 

JANUARI mwaka huu Mwekezaji  katika lilkilokuwa shamba la Shirika la kilimo na chakula nchini (NAFCO) kampuni ya kilimo cha mpunga cha Kapunga, aliridhia hekta 1,870 za ardhi zirejeshwe kwenye himaya ya kijiji cha kapunga.

Kurejeshwa kwa ardhi hiyo kulikotangazwa rasmi kwa wananchi kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kumeanzisha upya mahusiano ya kutegemeana kati ya wanakijiji na kampuni hiyo, mahusiano ambayo kwa miaka takribani 11 yalikuwa ya kusuasua na kutishia kukua kwa kilimo cha mpunga katika maeneo hayo ya Kapunga yaliyopo katika bonde la mto Usangu, wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Kurejeshwa kwa ardhi hiyo ambayo ilionekana kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa wa kutokuelewana kati ya uongozi na shughuli za kilimo kapunga na wanakijiji waliohamia hapo kwa bahati mbaya na kuanzisha kijiji ndani ya shamba la Nafco kumeelezwa na wananchi kama hatua ya kumaliza sintofahamu ambayo iligubika uzalishaji wa mpunga.

Kuna masimulizi mengi kuhusiana na mgogoro wa Kapunga, lakini sehemu kubwa ya maelezo hayo yanakimbia kueleza ukweli halisi wa uwapo wa kijiji chenye pilika nyingi katika eneo ambalo awali lilikuwa shamba la serikali.

Imeelezwa kuwa serikali wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi chini ya Rais Julius Nyerere, Wajapan walikubali kufadhili mradi mkubwa wa kilimo katika eneo la Kapunga.

Na baada ya majadiliano na kijiji kilichokuwa katika eneo hilo , Nafco walipewa eneo la Kapunga ambalo lilikuwa na wananchi wanne ambao walilipwa fedha zao na kuondoka.

Sunil Tayir, muongozaji wa kampuni hiyo ya Kapunga anasema pamoja na mgogoro huo kabla wao hawachukua menejimenti ya shamba kulikuwa na mahusiano mabaya sana kati ya waendeshaji wa awali na wananchi wanaozunguka shamba hilo kubwa.

Mahusiano hayo mabaya yalionekana wazi hata katika mambo ambayo hayakuwa na manufaa kwa majirani.

Mwalimu Nyerere inaelezwa alitembelea eneo hilo katika miaka yake ya mwanzo na kuwaambia kwamba uwapo wa shamba hilo kubwa ni baraka nyingi.

Ingawa baada ya kuuzwa kwa shamba hilo kulikuwa na migogoro mingi, neema imeonekana miaka zaidi ya mitatu sasa kiwango cha uzalishaji kimekuwa juu kufikia tani sita kwa hekta.

Aidha wakuliwa wadogo wanaopata nafasi ya kufanya kilimo cha pamoja katika maeneo yaliyotengenezwa tayari na kampuni wanajivunia mpango mahsusi wa kuwasaidia kulima ambao umewapa matunda sana.

Katika vitabu na katika maeneo mbalimbali kuna simulizi nyingi kutoka kwa watu wa rika mbalimbali katika eneo hilo la Kapunga wanaozungumzia Kapunga na asili ya shamba la mpunga la Kapunga.

Pamoja na simulizi hizo zenye kugongana na wakati ukweli unabaki palepale, Kapunga  haukuwa mji wala kijiji, umejizalisha kutokana na kuendelea kuimarika kwa shamba la mpunga la Kapunga.

Wakati wa kipindi cha pili cha mwaka 2006 serikali ilitangaza zabuni ya kuuza shamba la mpunga la Kapunga lililokuwa likimilikiwa na Shirika la NAFCO .

Pamoja na mwekezaji kununua shamba hilo huku makubaliano yakiwa ni kuzalisha chakula na pia kuwapatia maarifa wkaulima wadogo.

Lakini kutoka kipindi walichonunua hadi 2011 pamoja na kujaribu kuendeleza shamba hilo, kumefumuka migogoro iliyochelewesha sana maendeleo makubwa ya eneo hilo.

Mmoja wa wafanyakazi wa shamba hilo Sunil Tayir anasema kwamba iliwachukua muda mrefu katika kuhangaishana na wananchi waliokuwa wamekaa eneo hilo la shamba kwa sababu mbalimbali.

Katika mazungumzo na diwani alisema kwamba wanakijiji wa Matebete ndio wenye haki na eneo hilo kwa kuwa ndio walikuwa wametoa kibali kwa serikali kuchukua nafasi hiyo.

mwisho