Mhandisi wa Umwagiliaji mkoa wa Tabora matatani

TABORA: 14.01.2021

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiaji kumpangia kazi nyingine Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Tabora baada ya kushindwa kusimamia skimu ya Umwagiliaji Inala na maeneo mengine mkoani humo.

Hatua hiyo inatokana na udhaifu uliojitokeza katika Skimu Inala , Manispaa ya Tabora ya wakulima kulima ekari 15 badala ya hekta 400 zinazotakiwa kulimwa kwa msimu.

Bashe alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za miradi ya kilimo ukiwemo wa skimu ya umwagiliaji Inala iliopo Manispaa ya Tabora.

Alisema Mhandisi huyo Bahati Balekele ameshindwa kusimamia Skimu hiyo ya kuhakikisha kuwa wanakuwa na uongozi imara ambao utawasimamia wanachama ili walime kwa kiwango kilichokusudia kwa ajili ya kuleta tija ya mradi.

Naibu Waziri huyo alisema inasikitisha kuona kuwa Serikali imewekeza kiasi cha sh bilioni 2 lakini hadi kufikia jana ni ekari 15 ndio zilizokuwa zimelimwa na hivyo ikionesha wazi kuwa uwekezaji mkubwa wa fedha za umma haujaonesha tija.

Bashe aliongeza zipo baadhi ya Skimu mkoani humo ambazo zenye kasoro ndogo ndogo lakini Mhandisi huyo ameshindwa hata kuwahamasisha wakulima waweze kuchangia fedha kwa ajili ya kurekebisha kasoro ili ziendeleze kuzalisha kwa tija.

Kufuatia kasoro katika skimu ya Inala alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala ndani ya wiki mbili kuitisha mkutano wa wakulima wote kwa ajili ya kuchagua uongozi utakaosimamia mradi na kuwapanga wakulima katika mashamba mbalimbali ili waweze kuzalisha kwa tija.

Alisema katika mkutano wakulima wote wapangwe upya katika mashamba ya mradi huo na walime na atakayeshindwa kujitokeza atakuwa amepoteza sifa ya kupata eneo la kulima mpunga katika mradi huo.

Bashe alisema pamoja na mkutano huo ni vema Mkuu huyo wa Wilaya akaangalia uwezekano wa kuandaa taratibu za kuondoa tatizo la watu wawili ambao wamejimilikisha ekari 200 katika eneo la mradi.

Wakati huo huo Bashe amezitaka Halmashauri Mkoani Tabora kuhakikisha wanatenga maeneo makubwa ya kilimo( Block farm) kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali.

Alisema hatua itaziwezesha Halmashauri kuongeza mapato ya ndani ambayo yatawawezesha kujitegemea kwa asilimia mia moja.

“Halmashauri mkiwa ‘serious’ mtaweza kuanzisha block farm za mazao mbalimbali …hatua hiyo itawasaidia kupata fedha nyingi na kuacha tabia ya kufukuza na mamalishe na machinga kutafuta ushuru…mnapokuwa na block farm ni rahisi kwa mtu hata kuwekeza katika kiwanda kwa kuwa mwekezaji atapata malighafi katika eneo moja na kwa wingi” alisisitiza.

Bashe alisema badala ya Halmashauri kukimbilia katika upimaji wa viwanja  hata katika maeneo yanayostahili shughuli za uzalishaji wa mazao ni vema wakatenga mashamba makubwa kwa ajili ya kilimo cha korosho, alizeti, karanga , miembe na mazao mengine ambayo yatawawezesha wakulima kuwa na kipato kikubwa.

Alisema hatua hiyo itawasaidia wakulima kuondokana na kilimo cha kimazoea cha kuzalisha mazao kwa ajili ya kuijikimu na kuwa na kilimo cha uzalishaji kibiashara na Halmashauri kupata mapato yake.