Bil 130/- za korosho zaingia katika mzunguko Lindi

NACHINGWEA 18.1.2021

BAADA ya minada 23  mkoa wa Lindi umefunga rasmi msimu wa korosho 2020 na kuanza kujiandaa na msimu wa ufuta.

Msimu huo umemalizika baada ya kufanyika kwa mnada wa mwisho kwa wakulima wa Liwale kupitia Chama Kikuu cha Ushirika cha Ruangwa, Nachingwea na Liwale (Runali).

Mnada  huo wa 13 kwa Runali  ni mnada wa  23 kwa mkoa huo na ziliuzwa kilo 274,000 kwa bei ya shilingi 1,594 huku korosho tani 240 za daraja la pili ziliuzwa kwa kwa shilingi 1,367 kwa kilo

Zaidi ya Bilioni 130 zimeingia katika mzunguko wa wakulima wa korosho msimu huu 2020 uliomalizika.

Mnada  huo uliosimamiwa na Bodi ya korosho Tanzania na Ofisi ya Mrajis Msaidiz wa Ushirika mkoa wa Lindi  ulifanyika  mjini Nachingwea  na wazabuni  wawili walihitaji kilo 544,000 kupitia mfumo wa mauzo ya mtandao (TMX) huku sanduku likikosa wanunuzi.

Mrajis Msaidizi wa Ushirika mkoa wa Lindi,  Edmund Masawe akizungumza na HabariLEO alisema ameridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji,Mauzo na malipo ya haraka kwa Wakulima.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu (Runali), Hassan Mpako aliwapongeza wakulima,watendaji wa Amcos na Chama Kikuu kwa kukamilisha msimu bila dosari za malipo na upungufu wa vifungashio .

Mkulima wa wilaya Nachingwea, Hassan Mtoi, akielezea minada ilivyokwemda msimu huu alisema kwamba safari hii Runali wamewezesha bei nzuri na pia malipo kwa wakati kwa wakulima wa korosho.

“Kitu nilichofurahishwa nacho sana msimu huu ni namna ambavyo wakulima hatukupata usumbufu kuanzia vifungashio hadi malipo yetu  kinyume na misimu iliyopita” alisema Mtoi.

 Naye Mohamed Mbewile alisema kwamba mpaka wanamaliza msimu bei imekuwa sauti kubwa kwao na wamefurahishwa namna minada ilivyoendeshwa na malipo yao yalivyoshughulikiwa.

Pamoja na kumalizika kwa msimu huo Mrajis Msaidizi wa Ushirika mkoa wa Lindi,  Edmund Masawe aliwataka wakulima kutumia fedha walizopata kufungua mashamba ya mazao chakula ili kujiwekea akiba nzuri ya fedha.

Alisema kwa kuwa na mazoa ya chakula, fedha za mauzo ya korosho zinaweza kufanyakazi nyingine bdaala ya kununua chakula.

Pia amewataka wananchi kuhakikisha kwmaba wanajiandaa vyema kwa msimu wa ufuta na baadae mbaazi.