Watakiwa kuzalisha mbolea bora yenye bei nafuu

Babati

28.08.2020

Serikali imeviagiza viwanda vya mbolea nchini kuzalisha mbolea yenye viwango vya juu vya ubora na kuiuza kwa wakulima kwa gharama nafuu ili uzalishaji wa mazao uwe na tija na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kaya na taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alitoa agizo hilo leo mkoani Manyara alipotembelea kukagua kiwanda cha mbolea cha Minjingu.

 “ Nimeamua kufanya ziara hii kutembelea viwanda vya mbolea na kuongea na wazalishaji ili kuhamasisha upatikanaji wa mbolea yenye virutubisho bora na itakayouzwa kwa bei nafuu kwa wakulima nchini” alisema Kusaya

 “ Lengo la serikali ni kumkomboa mkulima, lakini hatuwezi kufikia lengo hilo kama mbolea itaendelea kuuzwa kwa bei kubwa nchini.Ndio maana tunataka viwanda vijengwe hapa nchini “ Kusaya alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema mahitaji ya mbolea nchini ni zaidi ya tani 664,000 wakati uzalishaji kwenye viwanda vyote 12 umefikia tani 38,000 pekee kwa mwaka.

Akizungumza kuhusu changamoto za kiwanda cha mbolea Minjingu kuwa na uzalishaji mdogo, Meneja Masoko wake Franks Kamhabwa alisema kiwanda kina  uwezo wa kuzalisha tani 100,000 za mbolea kwa mwaka kutokana na akiba ya madini ya fosfate takribani tani  milioni 8 hadi 10 kwenye mgodi wake lakini sasa hivi wanazalisha tani 23,598 kwa mwaka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Minjingu, Tosky Hans aliishukuru serikali kwa kukiunga mkono kiwanda hicho hali inayojidhihirisha kupitia viongozi mbalimbali kuizungumzia vizuri mbolea ya Minjingu.

Hans alimweleza Katibu Mkuu huyo wa Kilimo kuwa malengo ya kiwanda cha Minjingu ni kufikia uzalishaji wa tani 500,000 ifikapo mwaka 2025 na kuwa wataanzisha mashamba ya majaribio (Demo plots) katika halmashauri mbalimbali ili zitumike kufundishia wakulima juu ubora wa mbolea ya Minjingu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Dk Stephano Ngailo aliyeambatana na Katibu Mkuu kwenye ziara hiyo alimshukuru kwa kazi kubwa aliyoifanya kutembelea na kuhamasisha wazalishaji mbolea kwenye mikoa mitano.

Mwisho.